Serikali yamaliza mgogoro KIU

BAADA ya wabunge wa upinzani kuvalia njuga mgogoro kati ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala, Dar es Salaam (KIU-DCC) Kitivo cha Sayansi za Afya wanaosoma Kozi ya Famasia, serikali imefanikiwa kumaliza mgogoro huo na kuahidi wanafunzi wote watasajiliwa. … (endelea).
Serikali imewataka wanafunzi wote ambao walirejeshwa nyumbani kurudi chuoni ili kuendelea na masomo kwa kuwa mgogoro huo umepatiwa ufumbuzi.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Dk. Shukuru Kawambwa-Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Dk. Seif Rashid ambaye ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii wasema, wamekubaliana kumaliza suala hilo la usajili wa kitaaluma na kitaalamu katika tasnia ya ufamasia.
Waziri Rashid amesema, mgogoro umetatuliwa katika maeneo matatu ambayo ni usajili wa wahitimu wa programu za Astashahada na Stashahada za Famasia.
“Itakumbukwa kwamba, wanafunzi waligomea masomo kuanzia tarehe 13/4/2015 wakidai kutotambulika kwa astashahada, stashahada na shahada za programu za Famasia zinazotolewa na KIU ila baada ya majadiliano marefu tumefikia muafaka ambapo wanafunzi watapatiwa usajili kwa kufuata taratibu za kisheria,” amesema.
Amesema, mawaziri wote wawili wamekubaliana kumaliza suala la usajili wa kitaaluma na kitaalamu katika tasnia ya Ufamasia KIU-DCC, usajili wa wahitimu wa programu za astashahada na stashahada za famasia
Dk. Seif amesema, programu za kitaaluma za famasia zinazotolewa na KIU-DCC katika ngazi ya astashahada na stashahada zinatambuliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na wahitimu wa programu za famasia za KIU-DCC watasajiliwa na Baraza la Famasi kwa taratibu za kisheria.
Kuhusu taratibu za usajili amesema, zitahusisha ufuatiliaji na usimamizi kazini kama itakavyoratibiwa na Baraza la famasi na utambuzi wa wanafunzi wanaondelea na programu za astashahada na stashahada za famasia.
“Katika kukabiliana na changamoto kama hizo zilizotokea KIU kuanzia mwaka wa masomo 2015/16 wanafunzi wote watakaojiunga na masomo watafuata mtaala wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wenye ithibati ya NACTE,” amesema.
na kwamba, mtaala unaotumika na wanafunzi wanaoendelea na masomo ya Astashahada na Stashahada ya Famasia KIU-DCC utahuishwa ili uwiane na mtaala wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa lengo la kuwawezesha kusajiliwa na Baraza la Famasia watakapohitimu.
Dk. Rashid amesema, KIU-DCC kitatakiwa kudahili wanafunzi wa programu zote kwa kupitia Mfumo wa Udahili.
Kupitia changamoto zilizotokea kwenye mgogoro huo amesema, ipo haja ya kupitia sheria na kanuni zake kwa lengo la kuainisha majukumu, mipaka na maeneo ya ushirikiano. 
Amesema, kwa sasa wanasisitizwa kwamba Taasisi za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi  na zile za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zifanye kazi kwa kushirikiana kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Comments

Popular Posts