AMBULANCE’ NUSURA ICHOMWE MOTO SUMBAWANGA NA WANAINCHI.
Wananchi waliotaka kujichukulia sheria mikononi,
nusura walichome moto gari la wagonjwa
lilitolewa msaada Kituo cha Afya Mtowisa
wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa kutokana
na madai ya kuchangia kifo cha mwalimu mmoja
aliyekosa msaada wa haraka wakati wa
kujifungua.
Wananchi hao wanadaiwa kulishambulia gari hilo
kwa mawe na kuvunja moja ya kioo.
Gari hilo linadaiwa kuchelewa kuja kumchukua
Mwalimu Leah Mgaya wa Shule ya Msingi
Mtowisa 'A', ambaye alifariki baada ya kutokwa
na damu nyingi wakati wa kujifungua.
Habari kutoka sehemu ya tukio zilizothibitishwa
na Ofisa Tarafa ya Mtowisa, Peter Masindi
zinaeleza kuwa, awali mwalimu huyo alipelekwa
katika kituo hicho cha afya juzi saa 3 asubuhi
akiwa katika hali uchungu wa kujifungua, lakini
baadaye ilionekana anahitaji kupewa rufaa
kwenda Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini hapa.
Masindi alisema kutokana na hali hiyo ililazimu
kupiga simu Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya
saa 6 mchana ili kuomba msaada wa gari, lakini
gari hiyo ilichelewa kufika kutokana na kudaiwa
ilisafiri kwenda wilayani Nkasi, na hata iliporejea
jioni ilikwama njiani kutokana na hali ya mvua.
Mmoja ya wananchi waliozungumza na gazeti
hili, Mwaipungu alisema kifo cha mwalimu huyo
kiliwakera wananchi wa eneo hilo, ambapo
walikusanyika kwenye makundi na kuanza
kujadiliana.
Wananchi hao walidai kuwa gari hilo la
wagonjwa halina msaada kwani muda mwingi
haliko kituoni hapo hivyo kutaka kulichoma
moto.
Hasira za wananchi hao zilionekana baada ya
kufika kwa dereva wa gari hiyo aliyefika, huku
akiliza king'ora lakini alipokelewa kwa mabango,
kabla ya kumsimamishwa kumtaka kuwapa
funguo za gari, jambo lililopingwa na dereva.
huyo huku wananchi hao wakilishambulia kwa
mawe.
Comments
Post a Comment