Jambazi tishio kwa wanawake Arusha auawa

Arusha. Jeshi la Polisi mkoani Arusha
limefanikiwa kumuua jambazi aliyekuwa
akiutikisa mkoa huo kwa matukio ya kuteka
na kuwapora wanawake wenye magari na
kisha kuwapiga risasi.
Mtu huyo aliyefahamika kwa kwa jina la
Ramadhan Abdallah Jumanne maarufu kama
Rama Ndonga (37) Mkazi wa Moivo hatimaye
ameuawa polisi baada ya kupigwa risasi
katika majibizano na askari wa jeshi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha, Liberatus Sabas alisema jambazi huyo
aliuawa usiku wa kuamkia jana majira ya saa
2:04 usiku katika Kijiji cha Moivo, Kitongoji
cha Enaboishu wilayani Arumeru.
Alisema baadhi ya matukio ya ujambazi
aliyowahi kuhusika nayo ni lililotokea Agosti
6 mwaka huu saa 3:30 usiku maeneo ya Kwa
Iddi ambapo walimpiga risasi sehemu ya
shingo mwanamke Shamimu Rashid
aliyekuwa Mkazi wa Sakini wakati akijiandaa
kuingia nyumbani kwake na kumuua.
Kamanda Sabas alitaja tukio lingine ni la
Agosti 21 mwaka huu majira ya saa 1:00 huko
maeneo ya Olasiti, jambazi huyo akiwa na
mwenzake kwenye pikipiki walimjeruhi kwa
kumpiga risasi ya mdomoni na kutokea
kichwani mtoto Christen Nickson mwenye
umri wa miaka mitatu na nusu na kisha
kufanikiwa kupora Sh200,000 na baadaye
majeruhi huyo alifariki dunia akiwa
anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mount
Meru.
Aidha, kukamatwa kwa jambazi huyo ni baada
ya polisi kutumia mbinu za kisasa na kufika
nyumbani kwa marehemu na polisi
walimwamuru ajisalimishe lakini alikaidi na
kuanza kuwarushia risasi hali iliyosababisha
askari kujibu mapigo na hatimaye
kusababisha kifo chake.
Alisema kuwa, baada ya upekuzi mwili wa
marehemu ulipatikana na bastola aina ya
Glock 19 yenye namba RLU 976
iliyotengenezwa nchini Australia ikiwa na
magazine yenye risasi 14 ambayo alikuwa
ameishika mkononi pamoja na maganda
matano ya risasi.
Aidha, upekuzi zaidi uliofanywa katika
chumba chake ulibaini magazine moja yenye
risasi 15 na magazine mbili zenye uwezo wa
kubeba risasi 30 kila moja, redio call moja
yenye nembo ya ITSS/UNICTR, pikipiki aina ya
Toyo Power King rangi nyekundu yenye
namba za usajili T 507 BSU.
Upekuzi zaidi ulibaini kofia ngumu ya
kuendesha pikipiki rangi nyekundu, plate
number ya pikipiki yenye namba T 805 CVD,
pingu moja, Glock Fab Defence moja na vifaa
vya kusafishia bastola pamoja na koti jeusi.
Kamanda Sabas alisema polisi wanaendelea
kumsaka mwenzake waliyekuwa wakitumia
naye pikipiki hiyo, ili kuweza kuutokomeza
mtandao huo ambao umekuwa tishio jijini
Arusha.
Kutokana na tukio hilo, watu walifurika kituo
cha polisi kushuhudia mwili wa marehemu
ambaye aliutikisa mji huo.

Comments

Popular Posts